MTOTO ATAKA KUMRITH MAMA YAKE,AMBAKA

             MAUAJI ya kinyama yametokea Iringa baada ya kijana Ambokile Mbwanji (28), mkazi wa Mkwawa katika Manispaa ya  Iringa, kumchoma kisu na kusababisha kifo cha Costantino Matatala (50), mchana wa Jumatano iliyopita.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mzee Matatala aliuawa alipokuwa akijaribu kusaidia kuamulia ugomvi kati ya muuaji huyo na dada yake, Anna Mbwanji, mama yake na pamoja na watu wengine wawili.
Wanafamilia hao walikuwa katika mgogoro mzito ambapo mtuhumiwa alikuwa akiwatuhumu kumzuia kumrithi mama yake mzazi baada ya baba yao kufariki dunia.
I
meelezwa kuwa kijana huyo aliyekuwa akiishi Sumbawanga, alirejea mjini Iringa mwaka 2009 ambapo alikuta taarifa za kifo  cha baba yake mzazi lakini hakuonesha kuguswa na msiba huo.
Baada ya siku chache alianza vituko na  kujigeuza kuwa yeye ndiyo baba katika  nyumba hiyo huku akitoa amri mbalimbali kama alivyokuwa akianya marehemu baba yake enzi za uhai wake.
Akizungumza na gazeti hili, mmoja kati ya wanafamilia ambaye ni dada wa mtuhumiwa, Anna alisema kuwa mdogo wake Ambokile alijigeuza kuwa baba wa familia kwa  kumshurutisha mama yao mzazi ampe ‘huduma’ kama alivyokuwa akimpa baba yao, hali iliyosababisha familia kumkalisha kikao na kumkanya  juu ya tabia hiyo chafu.

Hata hivyo, alisema   katika tukio la wiki iliyopita, kijana huyo alivuta bangi na kunywa  pombe kupita kiasi tangu asubuhi hadi saa 8 mchana ambapo alifika sehemu mama yake anayofanyia biashara na kuanza na kutamka wazi  uhusiano anaotaka kati yake na mama yake.
Akasema asipokubali basi aanze kusali mara ya mwisho kabla hajamuua na ndipo alipomvamia mama huyo.
Anna aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, alilazimika  kukimbilia kituo cha polisi  kwenda kutoa taarifa lakini wakati anarejea, akapata habari kuwa mdogo wake tayari amemuua kwa kisu mzee Matatala.
Naye mama mzazi wa kijana huyo (Jina tunalihifadhi) alisema: “Kabla ya kumuua mzee huyo, alitaka kumuua kwa kisu mdogo wake wa kike na  wakati akimfukuza ili amchome kisu, alianguka na kisu kuvunjika.

“Akarudi na kwenda dukani kununua kingine kisha kurudi eneo la tukio akitaka kufanya mauaji lakini shemeji yake aliokota mawe na kuanza kumrushia hadi alipokimbia.”
Alifafanua kuwa kutokana na vurugu alizomfanyia na kelele nyingi zilizokuwepo sehemu hiyo, wakazi wa eneo hilo walijitokeza kutoa msaada, akiwemo Matatala na kuanza kumfukuza kijana huyo ambaye alikuwa na kisu mkononi huku wananchi wakipiga kelele za ‘mwizi’ na ndipo alipomchoma kisu mzee huyo.

Aliongeza kuwa, licha ya mzee huyo kuchomwa kisu, alimng’ang’ania kijana huyo hadi wananchi walipofika na kuanza kumshambulia kwa mawe na fimbo hadi alipopoteza fahamu na  kuja kuchukuliwa na polisi.
Akithibitisha kutokea kwa mauaji hayo, Diwani wa Kata ya Mkwawa,  Thobias Kikula amesema kuwa licha ya kijana huyo kumuua mzee huyo, bado alitaka kusababisha mauaji kwa  ndugu zake zaidi ya watatu, akiwemo mama yake mzazi na kuwa ushirikiano wa wananchi wa eneo hilo na jeshi la polisi ulifanikiwa kunusuru damu  zaidi kumwagika.

Ofisa mmoja wa polisi mkoa wa Iringa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema wanamshikilia mtuhumiwa licha ya kuwa amelazwa katika hospitali ya mkoa.

Comments