KATIKA PITIA PITIA ZANGU ZA MITANDAONI NIMEKUTANA NA MADA HII KATIKA MTANDAO HUU.. NAAAMI NIMEONA NIUKOPI KAMA ULIVYO ILI TU KUWAPA UTAMU WASOMAJI ....KAMA UTAPENDA UNAWEZA KUPITIA HUO MTANDAO HAPO JUU ILI UPATE MENGI ZAIDI MADA HII ILIANDIKWA NA Miki Da BataBoyz PrezDent
MWANAMUME yeyote anapotaka kumtongoza
mwanamke hulazimika kwanza kumwonesha – japo kwa matendo – kuwa
anampenda, au kwamba amevutiwa naye, hata kama ni kimwili tu. Hatua hii
ndiyo yenye changamoto kubwa zaidi kwa mwanamume, maana ndipo wakati
anapokuwa anajaribu kufikisha ujumbe kwa mlengwa huku yeye mwenyewe
akijihakikishia kuwa haharibu mambo.
Mwanamume anapokuwa anajaribu kufikisha ujumbe wa “nakupenda” kwa
mwanamke, mapigo ya moyo yanaweza kumwenda mbio, hususan kama mwanamke
mwenyewe anaonekana kuwa “maji marefu”. Hata hivyo, ni kazi ambayo kila
mwanamume hulazimika kuifanya.
Kazi hii ya kufikisha ujumbe kwa mara ya kwanza huhitaji umakini.
Bahati njema, shughuli yenyewe ina sayansi yake, ambayo ina misingi
katika mahusiano ya kijamii. Ukifahamu sayansi hii inaweza kuwa rahisi
zaidi kwako kufikisha ujumbe kwa mtarajiwa wako – na kufanikiwa.
1. KUKUTANISHA MACHO NI MUHIMU
Kawaida, mambo yote huanzia – na pengine kuishia – katika kukutanisha
macho. Mwanamke atakapobaini kuwa hujajaribu kumwangalia japo kwa
sekunde mbili mfululizo, ataondoa mawazo na hisia zake kwako hata kabla
hujasema neno lolote.
Macho ndizo zana muhimu zaidi mtu anapokuwa anataka kufikisha ujumbe
kwa mwenzake kuwa anampenda, au amevutiwa naye. Hii ni kwa sababu macho
ndiyo vipitisho na visambazaji muhimu vya ishara baina ya mtu na mtu,
hata kama si katika masuala yanayohusiana na mapenzi.
Kukutanisha macho na mtu wa jinsia nyingine unayevutiwa naye au
anayevutiwa nawe ni jambo lenye nguvu za ajabu katika kuanzisha
uhusiano. Kwa sababu hiyo, hata unapofanikiwa kumtazama moja kwa moja
machoni mwenzako hutarajiwi kutumia zaidi ya sekunde mbili, kutokana na
nguvu iliyomo katika mawasiliano haya.
Katika hili, wanaume mahiri hufahamu ni wakati gani wa kumwangalia
mwanamke na ni wakati gani wa kutomwangalia. Mara nyingi, ni vizuri
zaidi kumwangalia zaidi mwanamke wakati anapozungumza, huku ukikwepesha
macho kidogo pale unapozungumza wewe.
2. UNATAKIWA UWIANO, UKWELI KATIKA MAZUNGUMZO
Ni jambo lisilopingika kwamba wanaume na wanawake wanatofautiana
katika maana ya dhana ya mawasiliano. Hata hivyo, bado inawezekana
kuendesha mazungumzo shirikishi na yenye kuburudisha ukiwa na mwanamke,
bila kuonekana wa bandia.
Watu wa jinsia zote mbili wanaweza kutuhumiwa kwa kupindisha ukweli
na kujaribu kuficha tabia na mienendo yao wanapozungumza na wapenzi
watarajiwa. Naam, katika mazungumzo ya kwanza baina ya wapenzi au
wachumba watarajiwa uwongo – ukiwemo ule usiotarajiwa – huwa mwingi.
Katika mazungumzo ya kwanza ni kawaida kwa mwanamume kubadilisha
matendo yake na mtindo wake wa kuzungumza kwa maslahi ya kumpata
mwanamke, jambo ambalo huifanya hulka yake ya wakati huo kuwa ya bandia.
Lakini pia wasichana/wanawake husema “Nakupenda” bila kumaanisha,
pengine kwa ajili ya kumfurahisha mwanamume, au kusikia mwanamume
atasemaje.
Jambo la muhimu katika mazungumzo ya awali baina ya mwanamume na
mwanamke ni kuepuka michezo ya kudanganyana na kukwepana, badala yake,
yafanye mazungumzo kuwa rahisi na halisi. Hapo ndipo mwanamume
hujitofautisha na wanaume wengine na kupendwa kwa sababu hiyo.
3. USIPUUZE NGUVU YA LUGHA YA MATENDO
Wakati mtu anapokuwa akijaribu kuwasilisha ujumbe wa “Nakupenda” kwa
mwenzake, lugha ya matendo yake huzungumza kwa sauti kubwa zaidi kuliko
maneno yake. Hili limeweza kuthibitishwa kwa nyakati mbalimbali kutokana
na tafiti mbalimbali.
Katika muktadha wa kujaribu kufikisha ujumbe wa “Nakupenda” kwa
mlengwa, lugha ya matendo ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi. Kwa hakika,
asilimia kubwa ya ujumbe unaowasilishwa kwa mlengwa huwasilishwa kwa
njia ya matendo ya mwili na si maneno. Ni asilimia ndogo tu ya ujumbe
inayowasilishwa kwa maneno – na wakati mwingine maneno huweza kuleta
matatizo maana katika kuzungumza kuna kujikwaa kwingi, kwani ulimi hauna
mfupa.
Ili uweze kufanikiwa katika kueleza nia yako kwa mwanamke, lazima
ujue jinsi ya kutumia lugha ya matendo yako. Na pengine hutatumia nguvu,
maana watu husema penzi kikohozi – kama unalo litaonekana tu machoni pa
mlengwa.
Ukitafakari kwa makini utabaini kuwa huhitaji kusema sana ndipo uweze
kupendwa, kwani maneno huchangia asilimia kidogo tu. La muhimu ni
kuhakikisha kuwa mlengwa wako anakusoma na kukuelewa vizuri kwa
kuangalia matendo ya mwili wako.
4. ACHA ASILI ICHUKUE MKONDO WAKE
Katika nadharia mbalimbali za kijamii na kidini ni jambo la kawaida
kusikia kuwa binadamu wote ni sawa. Hata hivyo, katika muktadha wa
kimapenzi, kila mtu mmoja mmoja anafahamu kabisa kuwa si kila
mwanamume/mwanamke ni sawa na mwenzake.
Methali yenye asili ya kimagharibi husema “Uzuri wa mtu uko katika
macho ya yule anayemtazama.” Hii ina maana pia kwamba, kila mtu anavyo
vigezo vyake vya uzuri kwa kuzingatia maumbile yake. Pia jamii zinavyo
vigezo vya uzuri, lakini hutangulia kwanza vigezo binafsi.
Unapokuwa umekaa na mwanamke ambaye anakuvutia kwa mwonekano wake,
sauti yake na kadhalika, si rahisi sana kujizuia kuonesha kuwa
anakuvutia. Hii ni kwa sababu si wewe, bali ni nafsi yako inayokusukuma.
Na yeye mwenyewe atakusoma kwa kuangalia lugha ya matendo yako na
kukwelewa, utakaobaki ni uamuzi wake tu.
Katika jamii kuna vigezo kuhusiana na kiuno, miguu, maziwa, makalio
na kadhalika. Wengi wa wanajamii huvizingatia na kuongeza vyao. Huu ni
ukweli wa kibiolojia ambao hauwezi kupingika. Mwanamke mwenye vigezo
vinavyokubalika zaidi katika jamii yake atawavutia wanaume wengi zaidi.
Hapa mwanamume hahitaji kutumia nguvu nyingi – asili ya maumbile
itamsaidia humtambulisha mwanamke kuwa amempenda.
5. TUMIA CHANGAMOTO YA WALAKINI
Mara nyingi changamoto kubwa katika suala zima la mtu kubainisha nia
yake kwa mwanamke hutokana na ukweli kwamba katika mchakato mzima huwa
kuna wasiwasi na walakini. Kwa hakika, jambo hili ni la “pengine” au
“labda” kutokana na kutoweza kufahamu kirahisi mwenzako anawaza nini.
Unapoonesha nia yako ya kumpenda mwanamke, ni kama unaamsha hisia
zake kwako na ni kama vile unamuuliza: “Ungependa kuwa nami?” Kwa njia
hii ni kama utakuwa unafungua mlango wa kupata jibu la “ndiyo” au
“hapana” kwani huyo unayemwonesha kuwa unampenda na yeye ana matakwa
yake na mapendeleo yake.
Kimsingi hakuna kanuni wala sheria rasmi unazopaswa kuzingatia wakati
wote. La muhimu ni wewe mwenyewe kujiachia na kuingia katika maji
usiyofahamu kina wala mwisho wake, bali wewe nenda na mkondo wake huku
ukitarajia kuwa lolote linaweza kutokea. Hiyo ndiyo sehemu ya raha yake.
6. DHIBITI HISIA, MIHEMKO
Tofauti na mwanamke, mwanamume anayejaribu kuonesha nia yake hatakiwi
kujiweka katika mkao wa mwanamitindo. Wanawake ndio hufahamika zaidi
kwa mikao yao “ya kula” wanapokuwa katika mawindo (japo wengi hubisha),
lakini si mwanamume. Wanawake ndio hutarajiwa kujieleza zaidi kwa njia
ya matendo na mikao, lakini wanaume hutarajiwa kudhibiti hisia na
mihemko yao .
Tofauti katika lugha ya matendo baina ya watu wa jinsia mbili
hutokana na maumbile ya kujenetiki pamoja na utamaduni wa jamii husika.
Yote yakizingatiwa, matakwa ya mwanamke ndiyo hupewa kipaumbele zaidi.
Kwa ufupi, matendo ya kutongoza ya mwanamke huwa wazi zaidi, lakini
mwanamume hulazimika kuficha hisia na mihemko yake.
IFAHAMU SAYANSI HII
Wajibu wa kufikisha ujumbe kwa mtu wa jinsia tofauti ni wa kila mmoja
– mwanamume na mwanamke. Hata hivyo, wanaume ndio wenye jukumu kubwa
zaidi la kuanzisha, kwa kuzingatia utamaduni wa jamii nyingi. Unaweza
ukaona ugumu, lakini ipo sayansi itakayokusaidia. Kama una wasiwasi na
uwezo wako, ni vizuri kuyazingatia yote yaliyobainishwa hapa.