TFF-HAKUNA UCHAGUZI MKUU MARCH 2012!


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya Uchaguzi imefuta uchaguzi wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) uliokuwa ufanyike Machi 18.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo jana, Deogratias Lyato kamati yake imeamua kuufuta uchaguzi huo baada ya kukubaliana na ushauri wa kamati ya
Sheria, Katiba na Hadhi kwa wachezaji.

Juzi kamati ya Sheria, katiba na hadhi kwa wachezaji iliyo chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa ilitoa taarifa ya kuvitaka vyama vyote vilivyo chini ya TFF ambavyo katiba
zake zina mapungufu zifanyie marekebisho.

Katiba za vyama vyote wanachama wa TFF zinatakiwa ziendane na ile ya Shirikisho hilo na moja ya vipengele katika katiba ya DRFA ambavyo vinakinzana na hilo ni kipengele cha elimu ambapo itakiwa mgombea awe na elimu kuanzia kidato cha nne lakini ile ya DFA haisemi hivyo.

Taarifa ya Lyatto jana ilisema, “ Kutokana na mapungufu ya msingi ya Ibara ya 29 na Ibara ya 30 ya katiba ya DFA, kamati ya uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia katiba ya TFF Ibara ya 49 (1), katiba ya DRFA Ibara ya 48 na kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26 (2) kamati ya uchaguzi ya TFF kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba na kikanuni imefuta uchaguzi wa DRFA uliokuwa ufanyike tarehe 18 Machi, 2012…

“Mchakato wa uchaguzi wa DRFA utaanza upya mara baada ya kukamilika kwa marekebisho ya vifungu vya katiba ya DRFA vinavyokinzana na matakwa ya katiba ya TFF kwa maelekezo ya Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi kwa wachezaji kabla ya tarehe 10, Agosti, 2012”.

Aidha kamati hiyo ilisema kuwa kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 2 (4), uongozi wa DRFA utaendelea kuwepo madarakani hadi uchaguzi utakapofanyika kabla ya Agosti 10 muda wao wa kuwa madarakani kikatiba utakapomalizika.

Kwa muda mrefu katiba ya DRF imekuwa ikilalamikiwa na baadhi ya wadau kwamba ina upungufu mkubwa, ikiwa ni pamoja na suala la ukomo wa elimu, kuwepo kwa kipengele cha mgombea aliye madarakani kuruhusiwa kutetea nafasi yake bila kujali sifa za kikatiba.

Comments