Kemikali za sumu zilizoko katika tumbaku ya sigara huharibu DNA za mwili
wa binadamu dakika chache tu baada ya mtu kuanza kuvuta sigara. Kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, kemikali hizo zinazoitwa
Polycylic Aromatic Hydrocarbons (PAHs) husababisha DNA ziharibike na
kuongeza uwezekano wa mtu kupata kensa. Katika uchunguzi huo watalamu
walichukua kemikali hizo katika miili ya wavuta sigara na kuzifanyia
uchunguzi, ambapo waligundua kuwa, kemikali za PHA hubadilika haraka
mwilini na kuwa sumu ambayo huharibu DNA baada ya kupita dakika 15 hadi
30 tangu kuingia tumbaku katika mwili wa binadamu. Sumu hiyo hubadilisha
seli mwilini au kufanya mutation, kitendo ambacho huweza kusababisha
kensa. Wataalamu hao wanasema, kitendo hicho hufanyika kwa haraka sana
kama vile inavyoingizwa mada ya sumu kwenye damu kwa sindano.
Habari hii
ni tahadhari kwa watu wanaotaka kuanza kuvuta sigara, kwani takwimu
zinatuonyesha kwamba, watu 3,000 hufariki dunia kila siku umwenguni
kutokana na kensa ya mapafu, maradhi ambayo husababishwa kwa asilimia 90
na uvutaji sigara. Madhara ya kuvuta sigara kwa muda mrefu yanajulikana
na wengi, ambayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na kensa mbalimbali,
lakini wataalamu wanatuasa ya kuwa, madhara ya sigara huanza pale tu mtu
anapoanza kupiga pafu ya kwanza na kuingiza moshi wa sigara mwilini.
Hivyo bado hujachelewa na unaweza kuacha sigara hii leo!