UDSM KUSAIDIWA NA WB

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), huenda kikaongeza idadi ya wanafunzi wake katika mwaka mmoja ujao baada ya kupata msaada wa Dola42 milioni za Marekani, sawa na Sh65 bilioni, kwa ajili ya kuboresha miundombinu kutoka Benki ya Dunia (WB). Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mradi huo kwa makampuni ya wakandarasi, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Makenya Maboko alisema kuwa, UDSM imenufaika na mkopo huo kupitia Wizara ya Elimu, ambapo fedha za mradi huo zitatumika katika ujenzi wa majengo mapya, yakiwemo madarasa, ofisi na maabara. “Hatuna budi kuishukuru Benki ya Dunia kwa kufadhili mradi huu na hakuna shaka kuwa fedha zitatumika kama tulivyopanga,” alisema Profesa Maboko. Alisema kuwa chuo hicho kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa, ofisi na maabara na kwamba ujenzi wa miundombinu hiyo utakapoamilika utasaidia kupunguza msongamano na kuongeza idadi ya wanafunzi. Naye mtaalamu wa manunuzi wa mradi wa Benki ya Dunia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, John Kafuku alisema kuwa mradi huo utaomalizika baada ya miezi 12, unatarajiwa kutumia Sh27 bilioni kwa ajili ya ujenzi, Sh19 bilioni kwa ajili ya mafunzo ya wafanyakazi na nyingine kwa ajili ya vifaa vya ofisi. “Tunatarajia kujenga majengo saba, kusomesha wafanyakazi 56 katika kiwango cha shahada ya uzamili na uzamivu,” alisema Kafuku. Aliyataja baadhi ya majengo yanayotarajiwa kujengwa kuwa ni Kitengo cha Uhandisi, Sayansi Mchanganyiko, Sanaa na Sayansi ya Jamii, Uhandisi wa Madini na Elimu. Kuhusu wakandarasi waliopata zabuni ya mradi huo, Kafuku alisema kuwa kampuni nane za wakandarasi kutoka nchi za nje ndizo zilizopata zabuni hizo na mbili za wazawa.

0 comments:

Post a Comment

sema nasi hapa!!