HOTELI YA MATONYA YAGHARIMU TSH 150 ML

UKIANGALIA historia yake, hakika unaweza kusema amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kampeni za kuuaga umasikini.

Cha kufurahisha zaidi ni kwamba, ameyapata mafanikio hayo kupitia muziki wa kizazi kipya ambao katika miaka ya hivi karibuni umekuwa na mvuto, na pia ni `biashara’ kubwa kwa wanaoweza kuzichanga vyema karata zao.

Tunamzungumzia Seif Shaaban, maarufu kama Matonya ambaye baada ya muongo mmoja wa kupigana kisanii, sasa anaanza kula matunda ya kipaji chake. Leo hii, Matonya wa kwenye muziki ni `milionea’ fulani hivi.

Na umilionea wake hakuurithi, bali ameusotea, akadunduliza na sasa ana jeuri ya kuitwa Mkurugenzi. Anamiliki biashara kadhaa, ikiwamo ya kuuza magari, lakini sasa amekuja na kitu kipya, hoteli yenye hadhi ambayo iko mbioni kuzinduliwa, baada ya kumtafuna msanii huyo zaidi ya Sh milioni 150.
Matonya amethibitisha kuwa ndiye mmiliki wa hoteli hiyo iliyopo katikati ya Jiji la Tanga.

“Ni hoteli yangu, mali yangu iliyotokana na jasho la kazi yangu,” anasema mkali huyo ambaye aliwahi kuzushiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya na kukamatwa China, uzushi alioukana na kusema “sifanyi biashara hiyo, sifikirii kuifanya na wala sijawahi kukanyaga China”.

Anasisitiza kuwa, mafanikio yake yanatokana na kukuna kichwa na kutoa tungo na mashairi yenye hisia kali na mvuto kwa mashabiki wake, ndiyo maana ameweza kufanikiwa. “Tangu nianze muziki kazi zangu zimekuwa zikikubalika, nikaongeza idadi ya mashabiki wa ndani na nje ya nchi.

“Ndiyo maana kila kukicha nimekuwa nikipata mialiko ya kutumbuiza sehemu mbalimbali duniani, Ulaya, Marekani na hata Afrika nimezunguka,” anasema na kuhoji katika mazingira ya aina hiyo, kwa nini abaki katika maisha yale yale ya U-Matonya?

Anaongeza kusema: “Ndiyo maana mpaka hoteli yangu inafikia hatua hii, kila pesa imetoka mfukoni mwangu. Hata benki sijapiga hodi kukopa pesa ya biashara yangu hii ambayo natarajia kuizindua wakati wowote kuanzia sasa.”

Na wakati anajipanga kuizindua hoteli hiyo ambayo anaitafutia jina, Matonya yuko katika hatua za mwisho za kutoa kazi yake mpya kisanii, wimbo aliodai utakuwa gumzo unaoitwa Lesbian, yaani `Usagaji’. Katika wimbo huo, amewashirikisha wakali Abdul Naseeb `Diamond’ na Albert Mangweha `Ngwair’.

Kama ilivyo katika nyimbo zake zilizotangulia, nao umeangukia katika `mahaba’. Tofauti na mawazo ya wengi kuwa wasanii wanapaswa kubadilisha mwelekeo na kuachana na nyimbo za mapenzi, Matonya anasema nyimbo za mapenzi ndizo zinazouza.

“Kuna nyimbo nyingi za kusifia nchi, lakini hazifanyi vizuri sokoni ila nyimbo za mapenzi ndiyo zinauza,” anasema kijana huyo wa Kisambaa aliyekulia Barabara ya Tatu mjini Tanga. Miongoni mwa nyimbo za mapenzi zilizompatia umaarufu mkubwa Matonya ni pamoja na Anitha, Violeth, Taxi Bubu na nyingine kadha wa kadha.

Comments