MTANZANIA ASIMULIA ALIVYOPELEKWA MOTONI NA KURUDI TENA DUNIANI..INATISHAA SANA -02

Nikaenda kumfuata yule mtu, tulipofika mahali fulani na kutazama bondeni niliona bonde kubwa lililokuwa limefunikwa giza la kutisha mno.endeleea....


 Kabla ya kuwafikia wale
watu nilisikia sauti za watu zikilia kwa uchungu mkubwa mno, ndugu yangu kweli Jehanamu kuna vilio vya aina yake, vilio ambavyo huwezi kulia kama walivyokuwa wakilia wale watu, wanalia bila kupumzika. Lile giza nene mno linawafanya wale watu wasiwaze kutazamana kila mmoja na kilio chake na kila mtu na mateso yake hakuna mtu ayakayeondoka kwenda kumfariji rafiki yake, kwa sababu kila mmoja aliomboleza kwa ajili ya mateso yake, kadiri tulivyozidi kuteremka lile bonde ndivyo lile giza lilivyozidi kutoweka.

Ndipo tulipofika kule bondeni niliona watu wengi mno wasio na idadi; ni wengi kama weusi wa duniani, hakuna mzungu wala mwafrika wote ni weusi kupita kawaida. Na weusi uliosababishwa na baridi kali sana inayopatikana sehemu ile. Na ndimi zao zilikuwa zimevutwa hadi kufikia kila mtu kifuani pake, awe mrefu au mfupi. Nikauliza mbona ndimi zao watu hawa zinafika kifuani? Yule mtu akasema unavyoona sehemu hii haina maji wala haina furaha yoyote, sasa hizo ndimi wanazitumia kwa kulamba machozi, machozi haya hupatikana kwa kilio cha miezi mingi sana kupita na ndipo inatokea chozi moja ambalo hulitumia kama maji. Ndipo nikashikwa na uchungu wa ajabu nikakumbuka hawa ni watu walioishi chini ya Neema ya Mungu, lakini baada ya kufa kwao wako sehemu ya Jehanamu wakimsubiri baba yao aliyewadanganya. Kulikuwa na wanawake na wanaume.

Watu wale walikuwa wakilia kwa uchungu mkubwa mno. Nikamwomba yule mtu, nikisema Bwana naomba wachukue watu 100 kutoka kila nchi ili waone hii Jehanamu wawaambie wanadamu watageuka. Akasema wanadamu ni wenye mioyo migumu hata angerudi Yesu mwenyewe wasingemwamini wangeendelea na dhambi. Basi nikaendelea kulia sana. Kisha akaniuliza kama nilikuwa nawafahamu wale watu, nikasema siwafahamu. Akasema twende huku, nikaendelea kukatiza katikati ya mabilioni ya watu waliofia dhambi, kila mmoja na uchungu wake na kila mmoja na mateso yake.

Hata wa kwanza kumuona alikuwa Babu yangu mzaa Mama, yeye alikuwa ni Mwinjilisti na Mzee wa Kanisa katika kanisa la Lutherani kule Isapulamo Makete, sasa nilishangaa sana kumuona katika sehemu hii ya Jehanamu, yeye akiwa duniani alikuwa mweupe sana. Lakini sasa nilishangaa kumuona akiwa mweusi kupita kawaida. Nikamuuliza mbona mtu huyu alikuwa mtumishi wa Mungu na sasa namuona sehemu hii? Yule mtu akasema kweli kabisa huyu mtu alichaguliwa kwa ajili ya kazi ya Mungu lakini aliamua kuifanya kazi ya Mungu na kuingiza michanganyo. Na ndiyo maana ukamuona sehemu hii, ulevi kidogo alikuwa nao, ushurikina kidogo na mambo mengine kama hayo, kama maandiko yasemavyo Ufalme wa Mungu wanauteka wenye nguvu tu. (Matayo 11:12)

Mtu wa pili alikuwa jirani yetu, alikuwa ni kaka mmoja aliyekuwa anasali kanisa la Moraviani. Alikuwa ni kaka mmoja aliyejipenda sana na kila siku ya ibada na Jumapili alishika Biblia na kitabu cha nyimbo, kumbe alikuwa hafanyi mapenzi ya Mungu. Hata leo ukienda Uyole utasikia sifa zake. Huyu kaka alikuwa anaumwa sana na amelazwa katika hospital ya Mbeya, siku mbili kabla ya kufa kwake alituma watu kwenda kumuita mchungaji amwombee na baada ya siku mbili akafa. Sasa nikashangaa sana kumuona sehemu hii ya mateso, wakati huo huo wanasema mtu akiombewa anakwenda moja kwa moja mbinguni? Yule mtu akaniambia kawaambie watu wote duniani, mtu yeyote aliyejua kuwa dhambi ni mbaya na atakwenda Jehanamu, akisema nitatubu, nitatubu nikiona kwamba nimekaribia kufa, mimi huyo simpokei. Jinsi ninyi msivyopokea vitu vilivyooza ndivyo na mimi sivipokei japokuwa navitoa duniani (Ufunuo 22) Yule kaka akasema ninakuomba kawambie mama, baba na ndugu wasitende dhambi japokuwa mimi nimepata bahati mbaya kuja sehemu hii lakini kawaambie wasitende dhambi. Yule mtu aliyekuwa ananiongoza akasema usiende kuwaambia kwasababu duniani kuna wachungaji na waliookoka wanahubiri Injili wasipowasikia hao, nyumba nzima watakuja huku (Luka 16). Yule kaka akajitupa chini akalia kwa uchungu mkubwa mno.

Mtu wa tatu kunionyesha alikuwa Mama yangu mdogo upande wa Mume wangu (Alipokuwa anasafiri mme wake) akakorofishana na wakwe zake ( yaani wazazi wa mume wake) basi akanywa vidonge akafa, mume wake aliporudi na kuonyeswa kaburi mkewe akachukua vidonge akanywa sasa tulipokuwa tunaenda kwa rafiki yetu kumuona ndipo tulipishana na gari iliyokuwa inampeleka hospitali akiwa mahututi. Sasa nikashangaa sana kumuona katika ile sehemu ya mangojeo. Nikauliza huyu mtu niliyemwacha duniani na sasa namuona huku? Yule mtu akasema, kawaambie ndugu zake duniani, mtu anapokufa duniani ile sekunde moja tu, huku amekuwa ameshiriki kiasi cha kutosha, kama ni mtu wa uzima amekuwa na uzima na amekuwa mwenyeji, sasa huyu mtu hapa unavyomwona hata dakika kumi na tano hajamaliza. Nilishangaa sana maana alikuwa mweusi sana, ulimi wake umevutwa na kufika kifuani kama wale wengine. Alionekana kama mtu aliyekaa kwenye mateso yale zaidi ya miaka elfu kumi. Moyo wangu ulijaa huzuni na uchungu usio wa kawaida, basi yule mtu akaniambia sasa ‘kawaambie watu wote jinsi ulivyoona, na jinsi ulivyosikia usiongeze wala usipinguze atakayekataa usimlazimishe wala kumbembeleza, atakayekubari mwongoze sala ya Toba’.

Ndipo nikashangaa natokea katika nyumba ya yule rafiki yetu, wenzangu wote wametulia wakisubiri litakalotokea basi nikawaeleza yote niliyoyaona na kusikia basi tukamshukuru Mungu.

SURA YA 3

YERUSALEMU MPYA:

Siku ya tarehe 31/12/1991 niliongozwa na Mama kwenda shambani. Nilimweleza habari zote za baba yake, lakini mama hakuwa na la kufanya zaidi ya kusikitika, kwa maana nafasi ya baba yake ina gharama wala haina budi kuiacha hata milele (Zaburi 49:7-8)

Baada kufika shambani nilichimba shimo la kwanza, la pili na tatu kwa ajili ya kupanda mahindi, mara nikaanza kujisikia vibaya, basi nikamwambia mama akasema mwanangu hivi sasa ni saa tatu asubuhi watu wakikuona unarudi nyumbani watashangaa sana, vumilia kidogo. Sasa sikumbuki kama niliongeza kuchimba shimo au hapana. Nilishangaa niko kwenye sehemu nyingine ya tofauti kabisa na mazingira ya dunia, sehemu hii ilikuwa inaleta matumaini sana.

Sehemu hii ilinivutia mno basi nikawaza moyoni kama asipotokea yule mtu wa jana nitang’ang’ania huku huku. Nikaamua kukaa mara nikasikia sauti nyuma yangu ikisema ‘tufuate’ nilipogeuka nikashangaa kuwaona watu wawili waliofanana sana na mtu wa jana katika hali zote. Mmoja ameshika upanga na alisema anaitwa Mikaeli na aliyekuwa ameshika karatasi alisema alisema anaitwa Gabriel, Wasomaji wa Biblia wanajua kazi zao (Daniel 10:13, Yuda 1:9, Luka 1:26)

Nasikia sauti ndani yangu ikiniambia, inua macho yako utazame mbele nilishangaa sana kuona mbele yetu kulikuwa na nuru kubwa sana kutoka katika mji mmoja mkubwa na mzuri ajabu. Nuru ile iliangaza vizuri kuliko hata mwangaza wa jua na mwezi. Kwa kweli nilivutiwa sana na mji ule jinsi ulivyo na unapendeza. Nikauliza ule mji ni mji gani? Na ni kwa ajili ya nini? Wakaniambia ‘Ule ni mji Mtakatifu, Yerusalem mpya na ni kwa ajili ya Watakatifu walioshinda ya dunia’ Kwa kweli nashindwa hata kuelezea uzuri wa mji ule maana hauna mfano wa aina yoyote hapa duniani. Tumani langu ni kwenda kuishi katika mji wa utukufu mwingi sijui mwenzangu unatumaini gani?

Tulipofika mlango wa lile jiji, mawazo yangu yalinipeleka moja kwa moja katika tenzi namba 121 ‘’Liko lango moja wazi’’ Niliona lango moja kubwa lililokuwa wazi, (Ufunuo 3:7-8) lango hili lilikuwa likibadirika kila aina ya rangi, nyingine hazipo duniani. Tulipoingia ndani karibu na mlango tulimwona mtu mmoja mzuri sana mweupe na aling’aa sana, alikuwa amekalia kiti kizuri na cha thamani kupita kawaida. Alionekana kuwa mtu mpole mwenye huruma sana na upendo, (Mithali 11:28-30) tabasamu lake lilinipa raha ya aina yake na kuifanya nicheke sana kwa furaha na kujisahau. Malaika nilioongozana nao walianza kuzungumza na yule mtu kwa lugha nisiyoifahamu. Mimi nikaendelea kushangilia ule mji, ule mji umetengenezwa kwa vioo vitupu. Kila sehemu nilipotazama nilijiona mwenyewe (Ufunuo 21:18) nikaendelea kushangilia ule mji kwa uzuri wake na thamani yake hadi pale wale malaika waliponiambia tufuate.

Malaika walinitembeza mji mzima kwa muda mfupi sana hata sekunde moja haikuisha, nilishangaa sana sujui wametembea vipi wale watu. Malaika wa Kwanza akafungua mlango akaingia wa kwanza, pili nikaingia. Katika sehemu hii niliviona viti vingi sana vilivyokuwa vimeandikwa majina kwa damu mbichi. Vile viti vilikuwa vizuri na vya thamani kupita kawaida. Nikaomba kukalia kiti kimoja nikaambiwa utakalia ukishinda ya duniani.

Katika sehemu zote sikuona taa zikiangaza lakini kulikuwa na mwanga mzuri sana. Nikauliza mwanga huu unatokana na nini? Akaniambia mwanga huu ni wa mwanakondoo uliyemkuta mlangoni.

Nilipoingia kila mahali niliduwaa kwa kustaajabu ule uzuri wa mji ule. Kila mlango ulibadili baina ya rangi. Tukaondoka sehemu hii. Akafungua mlango mwingine nikastaajabu kuona bustani nzuri sana iliyozungukwa na maua ya majani yote yalikuwa na urefu sawa bila kuzidiana. Tena yalikuwa ya kijani kibichi sana. Maua ya sehemu hii marefu na yanamsifu Mungu kupita kawaida, yakiinama upande wa kulia yanakwenda yote na kusujudu na kuinuka hutoa harufu nzuri sana inayoenea mji mzima, maua hayo yalikuwa yamezungukwana kioo. Nikasema naomba nichume ua moja nikawaonyeshe ndugu zangu. Akasema maua ya huku hayachumwi, nikasema bustani hii imetengenezwa kwa hajili ya utukufu wa Mungu, nilitamani sana kukaa sehemu hii ya bustani, lakini wakasema tufuate.

Kila mahali tulipokwenda mmoja akafuata mwingine, nikasikia sauti nzuri mno zikiimba kwa furaha sana tukaingia, nikashangaa sana kuona watu wengi sana wasio na idadi. Nikajiuliza kwa nini Mungu anasumbuka kuwatafuta wanadamu wakati anao wengi sana? Nikastaajabu sana nikakumbuka pambio moja inayosema; Ukiringaringa kwa Yesu kuna watu wengi. Hawa watu walikuwa wanadamu kama sisi ambao waliishi duniani, lakini wao walimwishia Mungu na kufa na utakatifu.

Kama umewahi kuona mapacha basi wale ni mapacha wa aina yake. Sura zao hazitofautiani hata kidogo wamefanana sana hisivyo kawaida. Nywele zao zilikuwa ndefu wamezibana na banio jekundu sana, wala si wembamba sana na milifanikiwa kugundua tofauti moja tu. Wengine wamevaa mikanda miwili kiunoni na wengine mkanda mmoja. Nikauliza kuna tofauti gani kati ya waliovaa mkanda mmoja na waliovaa mikanda miwili? Akasema waliovaa mmoja ni wanaume na waliovaa miwili ni wanawake. Lakini ilikuwa sio rahisi kuwatofautisha kuwa huyu ametoka Taifa hili na yule Taifa lingine, waliimba wimbo mzuri isivyo kawaida, staili za uimbaji wao kwa kweli zilinifurahisha mno, walipunga mikono yao wote kwa pamoja na hapakuwepo hata mmoja wao aliyekosea. Nilipozidi kuwatazama nilitamani sana kujiunga nao ili nami niimbe na kumsifu kama wao wanavyosifu, lakini haikuwezekana kwa sababu hata lugha yao nilikuwa siijui. Baada ya muda akatokea dada mmoja na kuja upande wangu, niliweza kujua ni mwanamke kwa sababu alikuwa na mikanda miwili, nilishangaa kumuona yule dada kwa sababu niliweza kumtambua baada ya sura yake ile ya duniani kutokea. Yeye alikufa mwaka 1987 mwezi wa nne na aliuawa kwa kupigwa risasi. Yeye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari (Mbeya Day) kidato cha tatu (Form Three). Aliponifikia alisema ‘Ah Nyisaki, umekuha huku’ nikasema ‘Ndiyo’ akasema ‘Za duniani’ nikasema ‘Duniani matatizo’, akasema ‘Kweli matatizo. Angalia wenzenu tumevikwa miili mipya isiyoharibika, isiyopata magonjwa’ yaani aliusifu mwili wake na ni kweli ndivyo alivyo (1Korintho 15:40-53) akasema ‘Mwili wa zamani tumeuacha pale’, basi nikageuka niangalie amesema wapi, kweli ndugu yangu Biblia inasema mtafuteni Bwana maadamu anapatikana, mwiteni maadamu ya karibu (Isaya 55:6-7) mambo ya Uyole niliyaona kama vile unavyoweza kutazama kitu kwenye kiganja chako. Nilipoangalia sokoni nikaona biashara zinaendelea kama kawaida, barabarani magari na baiskeli ziliendelea kupishana kama kawaida, nilipotazama makaburini aliponionyesha huyu dada, nikaona makaburi ya watu wengi tena niliweza hata kusoma majina yao. Pia niliweza kujua wazi kabisa kuwa huyu yupo uzimani au jehanamu. Na kama hayupo ilionyesha wazi yuko uzimani. Kaburi la huyu dada lilionekana pia likiwa limepambwa maua. Akasema ‘umekiona kile kitu?’ Nikasema ndiyo, akasema ‘Ule ni mwili wako’. Kwa kweli sikupenda kuutazama mwili mara mbili, mwili wangu niliuona kama ngozi ya kenge chafu sana akaniambia geuka tena, nikakataa, mara ya pili nikakataa, mara ya tatu nikageuka nikaona kama mtu analima na kupanda mbegu akasema yule ni mama yako, fahamu zake tunazo huku, atarudishiwa fahamu utakaporudi wewe. Maono ya siku hiyo yalikuwa ya muda mrefu, kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni. Nilipochukuliwa kwenye maono mama alibeba mwili wangu kuweka kivulini, hapo ndipo nilitambua kweli fahamu zake zilichuliwa. Yule dada akasema Nyisaki kawaambie ndugu zangu wasitende dhambi tena katika mji huu hakuna huzuni, lakini ninawaona wanaendelea na dhambi nasikitika sana, wale Malaika wakasema ‘Usiende kuwaambia kule kuna walio’koka wanahubiri Injili, wasipowasikia hao basi ’

Mtu wa pili kunionyesha alikuwa mzee mmoja wa makamo aliyedharauliwa sana pale Uyole, alidharauliwa kwa sababu yeye alikuwa rafiki wa Biblia na Tenzi za Rohoni na kila alipojipumzisha iwe ni shambani, nyumbani au sehemu nyingine yoyote alisoma Biblia, aliimba Tenzi na kuomba, kweli yule alijishusha (Luka 14:35, 18:17, Isaya 51:7-8) watu walisema amechanganyikiwa. Nilishangaa kumuona katika sehemu hii akiwa kama kijana wa miaka ishirini (20), naye pia aliusifu mwili wake isivyo kawaida, kweli miili ile ni mizuri sana akasema kawaambie wapendwa wa duniani kila mmoja ajitahidi ashinde ya duniani maana muda umeisha, (Ufunuo 22:10-14) kila mmoja aangalie shetani asimpumbaze maana tuna hamu kubwa kuwaona wapendwa wetu, akaondoka akachanganyikana na wenzake.

Akatokea mtu wa tatu naye nilimtambua kuwa ni mwanaume kwa sababu ya ule mkanda mmoja, aliponikaribia ikatokea sura ya duniani, yeye alikuwa mzee wa Kipentekoste, alikuwa anasali Kanisa la Assemblies, akasema ‘Ah Chaula umekuja huku’ nikasema ‘Ndiyo’, ‘Za duniani?’ ‘Duniani matatizo’ akasema ‘Kweli matatizo, angalieni wenzenu tumevikwa miili mipya isiyosikia njaa, isiyopata magonjwa’ Basi aliusifu ule mwili, kweli alikuwa amebadirika naye alionekana kama kijana wa miaka ishirini (20) baada ya hapo akaondoka akaendelea kuimba. Baada ya kuonana na hao watu nikawauliza hao Malaika, hivi hawa watu wanajifunza kuimba? Wakasema kwa nini unasema hivyo, nikasema wanaimba wimbo hauishi akasema sivyo kama mnavyoimba duniani, maana duniani mkiimba dakika tano mnasema tumemsifu sana Mungu na wengine wanadhani wataenda mbinguni kwa sababu ya uimbaji bila kuokoka. Wimbo mmoja wa huku unaimbwa kwa miezi tisa, beti moja miezi mitatu, ‘’Chorus’’ miezi mitatu na beti ya mwisho miezi mitatu, basi nikashangaa sana. Tukaondoka hii sehemu akasema twende nikakuonyeshe watakatifu waliokuwako mwanzo wa kanisa, maana wameletwa sehemu yao akafungua mlango, tukaingia nikaonyeshwa watu kumi na sita (16), lakini nilijua wazi walikuwako na wengine zaidi

Mtu wa kwanza alikuwa Batholomayo, naye akanikumbatia na kunishika mkono, akasema Bwana ndiye aliyechunwa ngozi kwa sababu ya Injili. Na mtu wa pili kunionyesha alikuwa ni Yohana Mbatizaji, nikasema ndiye aliyekatwa kichwa kwa sababu ya Injili, akasema ndiye huyu. Basi akanikumbatia na kunishika mkono (Mathayo 14:1-11). Mtu wa tatu kunionyesha alikuwa ni Eliya Mtaabishaji wa Israel (1Wafalme 18:17-18) naye akanikumbatia na kunishika mkono, alinionyesha wengi sana akina Paulo, Petro na Yohana na wengineo. Batholomayo akasema, ‘Mpendwa, kawaambie wapendwa duniani, wakaze mwendo maana sekunde moja siyo muda mrefu’ (Filipi 3:12, 1Korintho 9:24-27), tukaondoka ile sehemu.

Wakanipeleka sehemu ambayo zinaandaliwa nguo za kuvaa watakatifu katika karamu ya Mwanakondoo, katika sehemu ile niliwakuta malaika wengi mno wakimsifi Mungu kwa shangwe. Katika sehemu hii pia kulikuwa na mashine nzuri zilizotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu mno, nguo nyingi sana ziliingia ndani ya mashine na kutolewa zikiwa zinang’aa sana, nikauliza mbona nguo zinatengenezwa nyingi sana, ni za nani? Maana watu wengi wanakataa wokovu. Akasema ‘Ninyi kaihubiri injili tu, anayetaka kuokoka na aokoke asiyetaka aache, kinachotakiwa ni kwamba anapokuja Mwana wa Adamu asiwepo wa kusema mimi sikusikia’

Basi tukaondoka ile sehemu. Ule mji ni sifa kila kinachofanyika, kilifanyika huku wakimsifu Mungu, si malaika wala si mwanadamu, si maua, si vinanda, maana vinanda vya kule vinapiga vyenyewe. Wakanipeleka katika ile sehemu ya awali iliyokuwa na viti vingi vyenye majina yaliyoandikwa kwa damu mbichi.

Tulipofika mara ya kwanza hakukuwa na mtu, lakini muda huu tulimkuta mtu mmoja aliyekuwa akifanya kazi kwa haraka sana, alikuwa amekazana sana kuliko Roboti. Nilimwuliza katika mji huu kuna watu wawili kama hawa? Tena kwa nini wamekazana sana hivi. Akasema huyu ni mtu mmoja kumbuka alipokuwa anaondoka duniani alisema, Ninakwenda kuwaandalia mahali ili alipo nanyi muwepo. (Yohana 14:1-6), akasema ‘huu mji ameuandaa mwenyewe hakuna mtu aliyemsaidia. Tena amekazana kwa sababu muda umefika wa kuchukua walio wake duniani’ (1Thesalonike 4:13-17). Wakaniondoa sehemu hii. Sehemu inayofuata ni sehemu muhimu sana, umesoma na kusikia zote za kwanza, sasa naomba utulie.USIKOSE SEHEMU YA 3 JUMATATU  IJAYO

SOMA  SEHEMU YA KWANZA  HAPA