MTANZANIA ASIMULIA ALIVYOPELEKWA MOTONI NA KURUDI TENA DUNIANI..INATISHAA SANA -01

 
MFANO WA ZIWA LA MOTO

UTANGULIZI:

Ndugu yangu kuna shuhuda nyingi sana zinazoanguka duniani, lakini wachache wanaozingatia kwa vile watoaji si wa dini zao au si wa madhehebu yao wala hawajulikani makanisani. Sasa ninakuomba ewe msomaji, tafuta mahali pa utulivu, mwombe Mungu na kusoma ushuhuda huu ili upokee kile ambacho Bwana amekuletea leo.

Msichana Nyisaki Chaula alionyeshwa na Bwana ushuhuda huu akiwa na umri wa miaka 16 mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Ushuhuda huu alionyeshwa akiwa ameokoka na si kwamba alikufa bali aliona maono. Maono haya alionyeshwa kati ya tarehe 30 – 31/12/1991; yaani kwa siku mbili tofauti.

Msichana huyu hivi sasa ameolewa na Mwinjilistii Lemsy Mheni pale Uyole Mbeya kwa lengo la kukuza huduma yao. Kabila lake ni Mkinga wa Makete, Msichana huyu anapatikana Uyole njia panda ya Malawi – Zambia na Dar es Salaam pembeni mwa kituo cha mafuta ya magari pale Uyole, Bwana awatangulie katika usomaji.

SURA YA 1

KUITWA:

Ilikuwa ni mwezi wa 12/1991 tulipochaguliwa vijana 10 kuombea Mkutano wa Kiroho ambao ulikuwa ukifanyika pale Uyole. Siku moja baada ya maombi ya usiku, nilala pamoja na dada zangu. Siku hiyo nilala usingizi mzito ambao sijapata kuona. Usiku nilishangaa kukuta usingizi umetoweka kabisa, hivyo nikabaki nikiwa macho, ndipo nikasikia sauti ikiita ‘Nyisaki’ nikasikia lakini sikuitikia, ikaita mara ya pili pia sikuitika. Hata mara ya tatu ndipo nikaitika kisha nikasikia ile sauti ikisema ‘Nimekuchagua kuwa mtumishi wangu’ ndipo nikatambua kuwa ni sauti ya Bwana, nikasema “Bwana mimi ni motto mdogo tena hata chuo chochote sijaenda nitawezaje kuifanya kazi hiyo? Bwana akaniambia mkumbuke Yeremia mtumishi wangu nilimchagua angali bado mdogo (Yeremia 1:5) basi nikaendelea kubishana na ile sauti hadi dada yangu mmoja aliamba na kusema ‘Mshukuru Mungu kwa sababu amekuchagua wewe’.

Ndugu msomaji kumbuka kuwa sauti hiyo nilisikia nikiwa macho kabisa na wala haikuwa ndoto na baada ya kusikia sauti hiyo mara ya pili na ya kwanza niliamka na kuthibitisha kabisa kuwa wote niliokuwa nimelala nao bado wamelala. Na hata huyo dada yangu alisema ‘Mshukuru Mungu kwa sababu amekuchagua wewe’ nilitambua kuwa ni Mungu ndiye aliyemuelimisha na kumfunulia jambo hili.

Baada ya yote haya tukamshukuru Mungu na kulala. Kesho yake tarehe 30/12/1991 ndipo nilipoonyeshwa mambo makuu ya ajabu (Yeremia 33:3)

JEHANAMU SEHEMU YA KWANZA NA MANGOJEO YA WAFU:

Ikiwa tarehe 30/12/1191 tulipoamka tukaenda kwenye semina na baada ya ile semina tuliamua kwenda kumuona rafiki yetu aliyeokoka ambaye kwa muda ule alikuwa hajiwezi yaani alikuwa anaumwa. Tulipofika pale nyumbani tukafungua ibada kwa maombi kisha tukaanza kujifunza jinsi Biblia inavyosema kwa njia ya maswali. Hata baada ya hapo tukaamua kufunga Ibada kwa maombi kama tukivyofungua.

‘Tufunge kwa maombi na kumkabidhi ndugu yetu mikononi mwa Bwana, maana tulianza ibada yetu kwa kumshukuru Mungu kwa kuwa ndugu yetu alikuwa hajambo’ Ninachokumbuka ni kwamba tuliimba pambio moja ya kuabudu lakini sikumbuki kwamba tuliingia kwenye maombi au la tulipokuwa tunaimba ile pambio ya kuabudu, nikashangaa kuona kuwa nimechukuliwa niko sehemu tofauti kabisa na mazingira ya nyumbani.
Ukiniuliza kuwa nilichukuliwa vipi hata mimi mwenyewe sielewi, lakini nilishangaa kuona kwamba niko kwenye bonde moja kubwa sana, na lile bonde lilikuwa halina miti wala majani wala ndege na vitu vilivyopo duniani, sehemu yenyewe ilikuwa haivutii hata kidogo, ni sehemu moja iliyokuwa na ukimya wa aina yake. Sasa nikashangaa mbona nilikuwa na rafiki zangu na sasa siwaoni, nikaendelea kujiuliza ni nani aliyenileta huku, na hapa ni wapi? Basi niliamua moyoni mwangu kuwa liwalo na liwe kwa sababu sijui hata aliyenileta mahali hapa, nilikuwa nimekata tamaa, nikajiandaa kutaka kukaa ndipo nikasikia sauti nyumba yangu ikisema ‘Nyisaki nifuate’. Nilipoinuka nilishangaa sana kumuona mtu mmoja mfano wa mwanadamu nilipomtazama yule mtu, umbo lake hakuwa mrefu sana wala hakuwa mnene sana, alikuwa ni mtu ambaye sijawahi kumuona popote duniani. Nywele zake zilikuwa ndefu na alikuwa amezibana nyuma kwa banio jekundu, alikuwa amevaa vazi refu mpaka miguuni na jeupe sana ambalo hata weupe wake sijawahi kuuona hapa duniani. Alikuwa ni mweupe sana, siyo weupe wa hapa duniani, macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, huyo mtu alikuwa hakanyagi chini bali alikuwa akitembea hewani na vazi lile lilikuwa liking’aa sana haliwezi kabisa kutazamika kwa macho ya binadamu. Nayasema mambo ambayo niliagizwa niyaseme, huyu mtu alikuwa amejifunga mkanda mmoja mwekundu kiunoni ndipo nikaamka nikaanza kumtuata. Baada ya hatua chache nikaanza kusikia muungurumo Fulani ambao ulinitisha kwa kiasi Fulani lakini sikuuliza. Kadiri tulivyozidi kutembea mbele ndivyo muungurumo ulivyozidi kuongezeka na kutisha zaidi, mara nikasikia sauti yangu ikiniambia inua macho na tazama mbele, ndipo nikashituka sana nilipoona moshi mkubwa mnene na mweusi umefunika bonde lile na kusababisha giza nene katika bonde. Nikamuuliza yule mtu huko mbele kuna nini? Yule mtu akasema, ‘hiyo ni Sehemu ya Jehanamu watakakoenda watenda dhambi baada ya maisha ya duniani’ Baada ya kusikia hayo yote ndiyo nguvu zikaniishia, nikaanza kulia na kumuomba sana Mungu anisamehe maana kwa mawazo yangu nilifikiri nimekufa na sasa napelekwa Jehanamu nikaendelea kulia sana hadi yule mtu aliponieleza usilie maana ukilia utashindwa kuwafikishia watu wangu habari hizi. Hofu ilijia nilitishika mno, lakini mpango wa Mungu kunionyesha mambo haya ni kuwaambia watu.

Ndugu msomaji, kweli Jehanamu ninavyoelezwa kuwa ni ziwa la moto elewa hivyo. Nilipotazama sikuona mwisho wake, bali niliona milipuko mikubwa sana na ya kutisha na milipuko hiyo haikufanana na milipuko yoyote hapo duniani labda kwa sehemu inayoweza kulinganishwa na milipuko ya visima vya mafuta.

Milipuko hiyo ni mikubwa na inatisha mno iliyosababisha moshi mkubwa sana ulioambatana na moto wa kupaa juu. Moto ule ulijichanganya changanya kama vile bahari iliyochafuka. Kulikuwa na mawimbi makubwa na ya kutisha na yakichanganyika na kutoa miungurumo mikubwa ambayo haiwezi kumfanya mwanadamu kusikia hata mateso ya mwenzake. Mimi nilipokuwa nasikia habari ya Jehanamu nilifikiri labda ni moto mdogo au makaa ya moto. Lakini siku hiyo niliyoona mwenyewe kiasi kwamba nilibaki kulia na kuomboleza kwa uchungu mkubwa mno. Mtu yule alifanya kazi ya kunionya nisillie, pia alinitia nguvu na ndipo nilipoweza kuendelea, ndugu yangu ukisikia Jehanamu iogope kama ulivyo.

Nilipoangalia ndani ya ule moto niliona vitu vyenye uhai virefu vyeupe nikauliza hivyo ni vitu gani? Yule mtu akasema ‘hao ni funza wa Jehanamu’ hizo rangi kwenye pingili zake ni za nini? Akasema hivyo siyo rangi, kama unavyowaona hao funza wana meno hayo manne yenye uwezo hata wa kutoboa fuvu la kichwa cha mtu, na huyo funza akishaingia ndani huacha sumu kali (yahani hiyo unayoiona kama rangi ambayo humtesa mwanadamu milele na milele.

Hao funza walikuwa ni wengi sana lakini hawafi ndani ya ule moto, (Marko 9:45-46) walikuwa wembamba warefu yapata mita moja, na walikuwa na pingiri pingiri ambazo zilionekana kuwa na rangi, walikuwa na meno mawili mbele na kichwani kulikuwa na meno mawili jumla ya meno yote manne, yaani mkiani na kichwani kulikuwa na midomo.
Bwana akasema ‘ hawafi wala hawaugui kwa sababu wamehifadhiwa kwa ajili ya mateso ya watenda maovu’

Ndugu msomaji, nisingeweza kupoteza muda wangu kukuletea jambo ambalo sijaliona lakini nimesema haya ili ukiwa na masikio na uyasikie, ukikataa ni juu yako mwenyewe. Maana sikuambiwa kwamba nimlazimishe mtu aokoke, bali niliambiwa nikamwambie kila mtu labda atakuwepo mmoja atakayegeuka na kuponywa. Sasa nikauliza mbona watu wanasema Jehanamu kuna wanaoungua lakini iweje Jehanamu hii haina watu wanaungua? Akasema wanasema kweli lakini watu watakuja kutupwa kwa wakati wake. Lakini muda huu wamehifadhiwa wakimsubiri baba yao aliyewadanganya (yaani shetani).

Akasema twende nikakuonyeshe nikaanza kumfuata. Kweli ndugu zangu Jehanamu uisikie kama ilivyo. Nilipofikiri habari za wale funza wa ajabu kwa kweli nililia kwa uchungu mkubwa mno nilitetemeka na kuishiwa nguvu nikaanza kuwaza moyoni mwangu mtu anayejua dhambi ni mbaya, na anajua neema ya Mungu na kupuuzia kweli uje kuteswa katika ziwa hili la kutisha lenye moto usiozimika na funza ambao hawafi, kwa kweli nililia sana. Lakini yule mtu akaniambai nyamaza, maana ukilia utashindwa kuyafikisha yote ninayotaka kukuonyesha. Kwa kweli nashindwa hata nieleze vipi. Jehanamu ni kweli ipo na inatisha sana; achana na mafundisho ya mashetani yanayosema hakuna Jehanamu na ukiendelea kufuata hayo utaangamia na kujuta milele. Ninaeleza ndugu yangu kuwa Mungu hapendi upotee ndiyo maana amekupa nafasi kama hii. Nayo yawezekana ni nafasi ya mwisho sasa usipokubali kutubu yawezekana ukajiletea maangamizi wewe mwenyewe.

JEHANAMU IMEANDALIWA KWA AJILI YA SHETANI NA MALAIKA ZAKE:

Niliondoka sehemu hii ya Jehanamu na kuelekea sehemu ya mangojeo nikiwa nalia kwa uchungu mkubwa mno. Na haya ninayokuambia sikutishi bali nakuambia kweli na kama unafikiri nakutisha basi utakwenda kuona mwenyewe.

Nikaenda kumfuata yule mtu, tulipofika mahali fulani na kutazama bondeni niliona bonde kubwa lililokuwa limefunikwa giza la kutisha mno.ITAENDELELEA  JUMATATU
(KUMBUKA KILA JUMATATU,JUMATANO NA  JUMAMOSI UTAPATA KUSOMA MKASA HUU WA KWELI UTAKAOBADILISHA MAISHA YAKO)

SEHEMU YA PILI SOMA HAPA SEHEMU YA PILI